MAMBO KUMI (10) MUHIMU YA KUZINGATIA KABLA YA KUNUNUA KIWANJA/ARDHI CHA KUJENGA
Wadau wa Ujenzi, nina wasalimia habari za wakati huu. Nimeona ni jambo zuri siku ya leo tujadili hasa mambo ya muhimu ambayo unatakiwa kuyafahamu ama kufanya kabla huja nunua kiwanja ama Ardhi kwaajili ya ujenzi wa nyumba yako. Hivyo basi kabla hujatafuta ardhi yoyote ni vema kuzingatia yafuatayo.
1. Eneo (location)
Hili ndio jambo la kwanza kabisa unalopaswa kuzingatia sana unapo taka kununua Ardhi ama kiwanja. Ni muhimu kujifuza tabia za eneo unalotaka kununua, fanya utafiti wa upatikanaji wa huduma mfano za elimu, afya, masoko na uwezekano wa usafiri kutoka eneo hilo kufika maeneo mengine ama ufikaji kwenye barabara kuu. Haya yata athiri sana maisha yako endapo huduma hizo zitakuwa hafifu ama hazitapatikana zitaongeza gharama ya maisha.
2. Ukubwa wa kiwanja (size of the plot)
Ukubwa wa kiwanja una maana sana wakati wa kununua kiwanja. Unahitaji kununua kiwanja ambacho kitaendana na uhitaji na ramani ya jengo lako. Hii itakusaidia kuwa na kiwanja chenye uwezo wa kubeba ramani ya jengo lako na kupata eneo la mashimo ya choo, eneo la ku paki gari na eneo la wazi kwa ajili ya kupumnzika na kujinafasi.
3. Hali ya eneo kisheria (status of the plot)
Hapa ni kuchunguza, kuuliza na kujua kama eneo hilo kisheria lipoje. Mfano lime pimwa ama halija pimwa?. Haya yatakusaidia kuwa na uhakika na unacho taka kukinunua. Maeneo mengi ambayo hayaja pimwa mara nyingi uhakika wa umiliki wake ni mdogo na mara nyingi hupelekea kwenye migogoro
4. Matumizi ya eneo hilo kwa ujumla (zoning and regulations/uses)
Haitoshi tuu kujua kwamba eneo hili limepimwa na ni eneo la makazi, ni muhimu kujua eneo linalo zunguka lina matumizi gani pia. Mfano unaweza kukuta umezungukwa na makanisa ama misikiti ama maviwanda, kitu hiki kinaweza kuathiri sana furaha yako katika kuishi kutokana na makelele na usumbufu mwingine.
5. Uwezekano wa majanga ya kimazingira (environmental hazards)
Ni vyema kuulizia na kufanya utafiti juu ya eneo unalo taka kununua kujua hali ya mazingira yake. Kwa mfano eneo kama lina historia ya mafuriko na mambo mengine yanayoweza kuhatarisha maisha yako sio zuri kwa matumizi ya kujenga nyumba.
6. Upatikanaji wa malighafi za ujenzi (availability of building materials)
Kufahamu kama eneo unalotaka kununua malighafi za ujenzi kama mchanga, cement, mbao na vitu vingine vina patikana? Na kama havipatikani je viki patikana kutoka mahala pengine panafikika? Kwa gharama gani? Hii itakusaidia sana kupunguza gharama zako za ujenzi.
7. Namna kiwanja kilivyo kaa (nature of the plot)
Namna kiwanja kilivyo kaa ina athari kubwa katika ununuzi wa kiwanja chako. Kwa mfano eneo lenye bonde sana lita kugharimu sana wakati wa ujenzi kwakuwa uta lazimika kutumia malighafi nyingi za ujenzi( kama tofali, mchanga, kokoto, nondo nk)wakati wa ujenzi ili kuhakikisha unapata jengo unalohitaji na katika uimara mzuri. Hii itakuongezea ghara(ma za ujenzi na kuathiri bajeti yako.
8. Bajeti yako ya fedha (budget)
Ni muhimu kufanya jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wako. Usijilazimishe kununua kiwanja cha gharama kubwa wakati ungeweza kupata cha gharama nafuu na pesa inayobaki ingekusaidia kuanzia huo ujenzi wako.
9. Hali ya Kijamii (Cultural/Social aspect of land)
Unapoamua kununua kiwanja, kinakuwa katika eneo ambalo watu wengine wanaishi na watu wa zamani pia waliishi au walifanyia shughuli zao hapo. Majirani watafahamu historia yake, ushirikina au mazingaombwe yanayofanyika hapo. Baada ya kumiliki kiwanja, wengi sana hufanya matambiko, kuleta wachungaji wafanye maombi au kupanda miti fulani ya kimila ambayo inakaribisha roho za mababu. Pia muhimu kuchagua aina ya majirani utakaowataka
10. Uwezekano wa kutengeneza pesa (financial capability)
Ardhi inapanda thamani kila baada ya muda. Uwezekano wa kuwekea dhamana katika mkopo, kuuza kwa haraka ikitokea shida, kupangisha ama kuiweka kama mali ya kampuni ni muhimu kuvitazam kwa mtu yeyote mwenye uchu wa kujiimarisha kiuchumi. Zaidi sana, kwenye ardhi inaweza kufanyika shughuli nyingi za kiuchumi kama kufuga, kulima ama kiwanda kidogo cha sabuni, mkate, mbao nk.
Ni wazi kwamba ukifanya makosa katika kuchagua kiwanja cha kujenga nyumba ya kuishi, utakuja kujutia. Ikumbukwe hapo ndio sehemu ambayo utahitaji kuishi kwa muda wako wote wa maisha ulio bakiwa nao hapa duniani hivyo ni vema ukawa makini sana na kufanya utafiti wa kutosha kabla hujaingia kichwa kichwa.
Ahsante kwa muda wako!